
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tamasha la Kizimkazi limekuwa sehemu muhimu ya kuchochea maendeleo ya Kizimkazi na Zanzibar kwa ujumla, kwa kuwa limeendelea kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na maendeleo ya wananchi.
Rais Samia amesema hayo wakati akifunga tamasha la 10 la Kizimkazi ambapo amefafanuwa kuwa , tamasha hilo limekuwa likiibua miradi ya maendeleo na kuwavutia wawekezaji pamoja na wageni kutoka ndani na nje ya Zanzibar, akieleza kuwa miradi mbalimbali iliyozinduliwa kupitia tamasha hilo inaakisi malengo ya kuunganisha shangwe, fursa na maendeleo kwa wananchi.

Amesema viongozi wanapaswa kuhakikisha fursa zinazopatikana kupitia tamasha hilo zinawafikia wananchi na kuwa na manufaa ya muda mrefu, ikiwemo kuboresha huduma za msingi kama maji, barabara na miundombinu mingine muhimu.
Rais Samia ameongeza kila mwaka tamasha hilo limekuwa likionyesha mabadiliko katika sekta mbalimbali, hivyo kuwahimiza wawekezaji na watu wenye nia ya kutumia fursa zilizopo kuendelea kuja Kizimkazi na Zanzibar kwa ujumla kuwekeza.
Aidha, Dkt. Samia ameitaka jamii, hususan vijana, kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini, akisisitiza kuwa amani ni chachu kubwa ya maendeleo na msingi wa wananchi kutumia fursa za kiuchumi na kijamii.

Rais Samia pia amewashukuru kamati ya maandalizi ya Tamasha la Kizimkazi pamoja na wazawa wa eneo hilo kwa ushirikiano waliouonesha katika kuwapokea na kuwahudumia wageni wakati wote wa tamasha.
Sambamba na hilo amewapongeza wadau na wadhamini walioshiriki katika kufanikisha tamasha hilo, pamoja na viongozi walioweka misingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono maono ya Tamasha la Kizimkazi katika kutangaza na kuenzi mila, silka na utamaduni wa Zanzibar.
Dkt. Mwinyi amesema taasisi za Serikali, wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wengine wamekuwa sehemu muhimu ya kufanikisha tamasha hilo, huku wazawa wakishiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika wakati wa tamasha.
Amesema Serikali itahakikisha tamasha hilo linatunzwa na kuendelezwa ipasavyo, sambamba na kuhakikisha miundombinu inayojengwa kupitia shughuli hizo inadumu na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Tamasha la Kizimkazi linaendelea kuwa chachu ya maendeleo si kwa Kizimkazi pekee, bali pia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kutokana na uwezo wake wa kuunganisha watu, fursa za biashara, utalii na uwekezaji.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amesema Tamasha la Kizimkazi limekuwa chachu ya maendeleo na limeibua fursa kwa wananchi katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, elimu, ajira, biashara na utalii.
Hamida amesema tamasha hilo lililofikia awamu ya 10 limeendelea kuwaunganisha wananchi na fursa mbalimbali za kiuchumi. Amesema wafanyabiashara 129 walisajiliwa kushiriki tamasha hilo, huku zaidi ya wafanyabiashara wadogo 200 wakinufaika na shughuli za kibiashara.
Amesema vijana wamepata fursa za ajira kupitia sekta ya utalii, wakati wavuvi nao wameendelea kunufaika na fursa zinazotokana na uwezeshaji wa shughuli za uvuvi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema tamasha hilo pia limeimarisha umoja na ushirikiano kati ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara, hivyo kuendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha watu, utamaduni na fursa za maendeleo.
Kwa upande wake, Haroun Ali Suleiman amesema jitihada hizo ni miongoni mwa matokeo ya uongozi wa Awamu ya Nane katika kuendeleza Kizimkazi na kuhakikisha wananchi wanapata fursa zinazotokana na shughuli za maendeleo na uwekezaji.
Tamasha la Kizimkazi 2026 limeendelea kuwa jukwaa la kuibua fursa za kiuchumi, kutangaza utalii, kuenzi utamaduni na kuchochea uwekezaji, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu na kutumia fursa zinazopatikana kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
...
📍 Wawekezaji waalikwa kutumia fursa za AFCON 2027
Na Beatus Maganja, Dodoma
...