TAWA YAWEKA MIKAKATI KUIMARISHA UHIFADHI NA KUONGEZA MAPATO
Na Beatus Maganja, Dodoma
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Yussuf Kabange, ameongoza kikao muhimu kilichowakutanisha Makamanda wa Uhifadhi wa Kanda, Makamishna Wasaidizi wa Ulinzi (ACC-P) pamoja na Maafisa Himasheria (APOs) kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika leo Aprili 26, 2026 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma, Kabange alisisitiza umuhimu wa kuimarisha udhibiti wa ujangili ndani na nje ya maeneo ya uhifadhi, pamoja na kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori (HWC) kwa kutumia teknolojia na kuongeza ushirikiano na jamii kupitia maeneo ya usimamizi wa wanyamapori (WMAs).

Katika hatua nyingine, alielekeza kuwa vitalu visivyo na wawekezaji vitumike kama fursa za kiuchumi, huku akisisitiza ulinzi madhubuti kwa vitalu vya uwekezaji, hususan SWICA, ili kuongeza mapato na kudhibiti vitendo vya uhalifu.
Kuhusu mapato, Kamishna huyo alihimiza kuendelezwa kwa vyanzo vilivyopo kama utalii wa picha, uwindaji na uvuvi, pamoja na kubuni vyanzo vipya na kuboresha miundombinu ili kufikia ongezeko la mapato la zaidi ya asilimia 13 kila mwaka.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeongeza bajeti kwa TAWA na kuonyesha imani kubwa kwa taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi. Hivyo, aliwataka viongozi na watendaji kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo Mpango Mkakati wa Shirika pamoja na Ilani ya Serikali.
Katika kusisitiza uwajibikaji, Kabange alielekeza kusimamiwa kwa doria kwa ufanisi, kuzingatia sheria, kuepuka vitendo vya rushwa, pamoja na kulinda usalama wa askari na wananchi kwa kufanya kazi kwa weledi, busara na utu.

Pia, kikao hicho kilijadili umuhimu wa kuanzisha miradi ya kiuchumi ikiwemo mashamba ya wanyamapori na bustani za wanyamapori (zoo) kama sehemu ya kuongeza mapato na kuimarisha uhifadhi endelevu



