TAWA yashiriki Mkutano wa Kimataifa wa Utalii Afrika
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Utalii Afrika uliofanyika Jijini Arusha mnamo tarehe 21/5/2024 ambao uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya African Queen Adventure, Travel Shop Turkey na International Ecotourism Society, ambapo ulihusisha mawakala wa utalii wapatao 120 kutoka nchi mbalimbali duniani zikiwemo Uturuki, Indonesia, Italia, Malaysia, Uingereza n.k

Dhima kuu ilikuwa kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania kwa mawakala wa utalii waliohudhuria mkutano huu.
Mkutano huu ulihusisha wadau mbalimbali wa utalii wakiwemo wazungumzaji wabobezi wa utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania pamoja na mawakala wa utalii ambao walifanya mazungumzo ya biashara (Business to Business Networking) na watoa huduma za utalii wa Tanzania, kisha kutembelea maeneo yaliyohifadhiwa kupitia safari za Mafunzo (FAM Trips).

Ushiriki wa TAWA ulihusisha kuuza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika maeneo inayosimamia kwa watoa huduma za utalii nchini Tanzania na mawakala wa utalii wa kimataifa. Kubadilishana uzoefu pamoja na kujenga mahusiano ya kibiashara na wadau wa utalii.




