TAWA YASHIRIKI MAONESHO  YA 52 YA KIMATAIFA YA UWINDAJI WA KITALII NCHINI MAREKANI

TAWA YASHIRIKI MAONESHO YA 52 YA KIMATAIFA YA UWINDAJI WA KITALII NCHINI MAREKANI

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeshiriki katika maonyesho ya 52 ya Kimataifa ya Uwindaji wa Kitalii yanayoratibiwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchini Marekani inayojulikana kama “Safari Club International  SCI”. Maonyesho hayo yalifanyika Jijini Nashville, Tennessee nchini Marekani kuanzia tarehe 31 Januari 2024 hadi 03 Februari 2024.

Ujumbe wa TAWA uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (mst) Hamis R. Semfuko akiambatana na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Bw. Mabula Misungwi Nyanda, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi - Huduma za Utalii na Biashara Bw. Fredrick Ligate na Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Matumizi Endelevu ya Wanyamapori - Arusha Bi. Lucy Lyimo.  

Kabla ya kushiriki katika maonyesho hayo, wajumbe kutoka Tanzania walipata nafasi ya kukutana na Mhe. Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Dkt. Elsie S. Kanza. Pamoja na kujitambulisha kwa Mhe. Balozi, wajumbe hao walijadili mambo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kushirikisha wadau wa ndani na nje katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uwindaji wa kitalii katika kuimarisha uhifadhi, kuongeza idadi ya watalii na mapato. Aidha, Mhe. Balozi alihaidi kuunganisha tasni ya uwindaji wa kitalii ya Tanzania na Mamlaka za Serikali ya Marekani. 

Tanzania ilipata nafasi ya kipekee ya kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Congress inayohusika na Maliasili (House Committee on Natural Resources Chairman) Bw. Bruce Westerman ambapo mambo mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani yalijadiliwa ikiwemo masuala ya uwekezaji katika sekta ya utalii na mchango wa tasnia ya uwindaji wa kitalii kiuchumi, kiikolojia na kijamii.

 Bw. Bruce Westerman aliahidi kuitembelea Tanzania mwaka huu 2024 ili kujionea juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza sekta ya Maliasili ikiwemo madini na nishati.

Washiriki kutoka Tanzania pia walipata nafasi ya kufanya kikao na Taasisi ya Marekani inayohusika na Usimamizi wa Masuala ya Uhifadhi wa Samaki na Wanyamapori (US-Fish & Wildlife Service - USFWS) na kukubaliana masuala mbalimbali ya kimkakati katika kuendeleza uhifadhi na uwindaji wa kitalii. 

Aidha, kikao hicho pia kilijadili suala la kushirikiana katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uwindaji wa kitalii ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana vikundi vinavyopinga matumizi endelevu ya wanyamapori ikiwemo uwindaji wa kitalii. 

Vilevile suala la uingizaji wa nyara za simba na tembo kutoka Tanzania lilipewa kipaumbele kwenye majadiliano hayo ambapo USFWS iliahidi kulipatia ufumbuzi suala hilo haraka iwezekanavyo ili kuendeleza mahusiano baina ya nchi hizi mbili.

Aidha, washiriki walipata nafasi ya kufanya mazungumzo na baadhi ya wamiliki wa kampuni za uwindaji wa kitalii zilizoshiriki katika maonyesho hayo na kujadili kuhusu mikakati ya kuboresha tasnia ya uwindaji wa kitalii kwa kuzingatia mahitaji ya soko na ushindani uliopo. Baadhi ya wamiliki hao walikiri kuwa hali ya soko la uwindaji wa kitalii kuanzia mwaka uliopita imeimarika na kwamba wamekwishauza hadi safari za mwaka 2026. 

Hata hivyo, baadhi ya washiriki hao walieleza kuwa gharama za uwindaji wa kitalii kwa Tanzania ziko juu ukilinganisha na nchi zingine. 

Vilevile, washiriki walipata fursa ya kufanya kikao na waandaji wa maonesho hayo (Safari Club International - SCI) na Safari Club International Foundation (SCIF) na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo uhifadhi na utafiti wa Simba na Chui. Kupitia kikao hicho, Tanzania ilipata nafasi ya kujadil masuala ya uhifadhi wa wanyamapori wakubwa jamii ya paka pamoja na mipango ya kufanya mapitio ya Mkakati wa kuwahifadhi wanyamapori hao.