TAWA YAJIPANGA KUIINGIZIA SERIKALI MAPATO MAKUBWA KUPITIA MAKUYUNI WILDLIFE PARK

TAWA YAJIPANGA KUIINGIZIA SERIKALI MAPATO MAKUBWA KUPITIA MAKUYUNI WILDLIFE PARK

Na Beatus Maganja

Makamu Mwenyekiti wa  Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Dr Simon Mduma amesema mpango mkatati wa kibiashara wa kuendeleza shughuli za utalii eneo la Makuyuni Wildlife Park uliondaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA unatarajiwa kuiingizia Serikali mapato makubwa ikiwa ni pamoja na kunufaisha jamii zinazozunguka eneo hilo

Dr Mduma ameyasema hayo Novemba 25, 2023 wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya TAWA katika hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park iliyopo wilaya ya Monduli , Mkoa wa Arusha ikiwa ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa bodi hiyo kufanya ziara katika hifadhi tangu ikabidhiwe kwa TAWA  Oktoba 03, 2023

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko, Dr Mduma amesema tangu eneo la Makuyuni Wildlife Park likabadhiwe kwa TAWA, menejimenti ya TAWA imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa mpango maalumu wa biashara na kuendeleza eneo hilo ili liweze kutumika vizuri kwa biashara ya utalii na mpango huo uliwasilishwa kwenye bodi na bodi ikaridhia utekelezaji wake

Aidha amesema pesa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ipo na imekwisha tengwa kilichobaki ni kuanza utekelezaji.

 Pia ametoa rai kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa eneo hilo kuongeza ushirikiano kwa TAWA kwa kuwa mradi huo ni wa Taifa na  umma kwa ujumla na wao kama wananchi wa eneo husika ni wanufaika wakubwa wa mradi huo

Kwa upande wake,  Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda  amesisitiza kuwa TAWA itahakikisha  inawashirikisha  wananchi wote wa Makuyuni katika shughuli zote zitakazofanyika eneo hilo, lakini kwa kuanzia TAWA itaanza zoezi la kuainisha mipaka  ili ijulikane kwa wananchi wote

Kamishna Mabula amesema katika eneo hilo kutakuwa na kazi nyingi zitakazofanyika ambazo zitawanufaisha wananchi hasa katika upande wa ajira kama vile ujenzi wa miundombinu  ya barabara, malazi ya watalii n.k

Aidha, amewapongeza wanahabari wote nchini kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutangaza utalii na  shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAWA nchini.

Naye Kamanda wa Makuyuni Wildlife Park Andrew Kishe amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa kukabidhiwa kulilinda eneo hilo hali ya usalama wa Wanyamapori imeimarika sana na kupelekea ongezeko kubwa la Wanyama hao.

Pia amewakaribisha wageni  wote nchini na nje ya mipaka ya Tanzania kutembelea eneo hilo kwa kuwa ni eneo la kipekee lililobahatika kuwa na mnyama adimu anayeitwa choroa "Oryx"