TAWA YAINGIZA NGUVU MPYA

TAWA YAINGIZA NGUVU MPYA

Askari wa Uhifadhi 256 waapa kulinda rasilimali za Taifa

Na. Joyce Ndunguru, Mwanza.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imehitimisha rasmi mafunzo ya Kijeshi kwa Askari wapya 256 katika hafla iliyofanyika katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi jijini Mwanza leo Februari 2, 2026.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Malisili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewataka Askari wapya kuwa watiifu na wazalendo katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori pamoja na kuzingatia sheria na haki katika utoaji wa huduma.

“Ni matumaini ya Serikali kuwa mafunzo mliyopata yamewapa ari na nguvu zaidi katika kuhifadhi na kulinda rasilimali za wanyamapori pamoja na kufanya kazi na kutoa huduma kwa watanzania wote bila kujali kabila, dini na jinsia”, amesema Dkt. Abbasi

Sambamba na hilo, Dkt. Abbasi amewaelekeza Askari hao kwenda kushirikiana na jamii katika shughuli za uhifadhi na kuhakikisha jamii pia inanufaika na uwepo wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo yao na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.

Kadhalika, Dkt Abbasi ameongeza kuwa Wizara imeendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi kwa kuandaa Sera, Mikakati na Miongozo madhubuti ili kuwezesha Jeshi la Uhifadhi kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amiri Mkalipa, amewaasa Askari wahitimu kuhakikisha wanatimiza majukumu watakayopangiwa kwa kufata misingi iliyowekwa na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen (Mst) Hamis Semfuko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha kuajiri Askari wapya 256 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii. 

Pia, ameongeza kuwa Bodi itawatumia kikamilifu Askari hawa katika kulinda rasilimali za wanyamapori kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Awali, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange amewapongeza Askari wapya waliohitimu mafunzo na aliwaelekeza Askari kwenda kutekeleza majukumu ya ulinzi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili na taratibu za kijeshi. 

Aidha, ameongeza kuwa TAWA itaendelea kutoa mafunzo kwa Askari ili kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanaendelea kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Akitoa salamu za ukaribisho, Mkuu wa Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, Jeremiah Msigwa amewashukuru TAWA kwa kuchagua Taasisi yake kwa ajili ya kuhitimisha mafunzo hayo, kadhalika amewataka wahitimu wote kuwa wazalendo katika kulinda rasilimali za wanyamapori.