TAWA NA WADAU WAKUTANA KUJADILI KANUNI ZA UTALII WA PICHA
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii leo tarehe 11.07.2024 imefanya kikao na wadau kwa ajili ya kupokea maoni kuhusu Kanuni za utalii wa picha (Non consumptive use) kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro Crater, Jengo la Ngorongoro jijini Arusha.

Kikao hicho kimefunguliwa na kuongozwa na Mkurugenzi wa huduma za Sheria wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Lucy Saleko.


Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Bi.Lucy Saleko alibainisha kuwa madhumuni ya kikao hicho ni kupokea maoni ya wadau juu ya marekebisho ya kanuni tajwa hivyo ni vyema kutoa mawazo yatakayowezesha kuweka mazingira wezeshi katika biashara.


"Tumekutana leo kwenye kikao hiki muhimu kitakachotoa mwelekeo katika tasnia ya Utalii wa picha kwenye maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania hivyo ni muhimu kila mmoja wetu kutoa mawazo yanayofaa ambayo yatawezesha kuifanya tasnia hii kuwa bora" alisema Bi. Saleko.


Kanuni za utalii wa picha zikitungwa mwaka 2016 na haikuwahi kufanyiwa marekebisho ingawa kumekuwa na mabadiliko mbalimbali katika tasnia ya Utalii wa picha hivyo kusababisha uhitaji wa marekebisho ya kanuni hii ili kuendana na mazingira ya wakati huu.






