RAIS SAMIA AIPONGEZA TAWA TAMASHA LA KIZIMKAZI ZANZIBAR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii hususan Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kutoa fursa kwa wakazi wa visiwa vya Zanzibar kuweza kuwaona wanyamapori hai katika tamasha la Kizimkazi lililofanyika paje Zanzibar.
Rais Samia ameyasema hayo katika kilele cha tamasha la Kizimkazi lililofanyika Agosti 31,2023 katika viwanja vya Kashangae, Paje, Zanzibar.

"Kwenye maonesho haya nawashukuru sana Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini kwa mahusus TAWA, kwa sababu kwa mara ya kwanza jamaa zangu hawa wa Kusini Unguja wamemuona simba "Live" (mubashara), wamezoea kumuona simba kwenye televisheni na picha, mara hii wameona simba jike na wameona simba dume "Live" (mubashara ) wako pale nyuma"

"... lakini wamemuona chui yuko pale, fisi yuko pale na pia wamemuona zebra yuko pale kwenye maonesho. TAWA ninawashukuru sana sana, mmetusaidia kutufungua macho wana Kusini" amesema Rais Samia.

TAWA imeshiriki kikamilifu katika tamasha la Kizimkazi kwa kuwapeleka wanyamapori hai kama vile Simba, Chui,Pofu,Pundamilia, Fisi madoa, Nungunungu na ndege mbalimbali ambao walikuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali waliotembelea tamasha hilo.






