KAMISHNA WA TAWA AKUTANA NA VIONGOZI WAPYA WA TWEA
📍 Wajadili mazingira ya biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai
✍️ Na Beatus Maganja, Morogoro
KAIMU Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Y. Kabange, Agosti 24, 2026 alikutana na viongozi wapya wa Chama cha Wafanyabiashara wa Usafirishaji wa Wanyamapori Hai (Tanzania Wildlife Exporters Association – TWEA) kwa lengo la kujitambulisha na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu biashara hiyo.
Viongozi hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Makamu Mwenyekiti na Katibu, walitumia kikao hicho kueleza utayari wao wa kuimarisha ushirikiano na Serikali kupitia TAWA, hususan katika kuweka mazingira yatakayowezesha biashara hiyo kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi wa wanyamapori.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zilijadili pia changamoto na vikwazo vinavyowakabili wadau wa biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai na namna ya kuvipatia ufumbuzi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mazingira bora ya uendeshaji wa biashara hiyo endapo itafunguliwa tena.
Aidha, TAWA na viongozi hao walibadilishana mawazo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wafanyabiashara ili shughuli hiyo itakaporuhusiwa, iweze kufanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria pamoja na misingi ya uhifadhi endelevu wa rasilimali za wanyamapori.
Kikao hicho kinaendeleza jitihada za Serikali za kushirikisha wadau katika kujadili masuala yanayogusa sekta ya wanyamapori, kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza na kujenga mazingira ya ushirikiano katika usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori.



