BONGOZOZO ASTAAJABISHWA NA UPEKEE WA MAPOROMOKO YA MAJI MPANGA/KIPENGERE
Na Beatus Maganja, NJOMBE
Balozi wa Utalii nchini na mwanamitandao maarufu duniani Nicholas Reynolds almaarufu bongozozo ameeleza kushangazwa na kufurahishwa kwake na uzuri na upekee wa vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Pori la Akiba Mpanga/kipengere.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 16, 2023 alipotembelea hifadhi hiyo katika ziara yake ya kuhamasisha na kutangaza vivutio utalii vilivyopo Kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuadhimisha siku ya maporomoko ya maji duniani ambapo Kitaifa yamefanyika katika Pori la Akiba Mpanga/Kipengere lililopo katikati ya mikoa ya Mbeya na Njombe.

"Nimetembelea maporomoko mengi sana hadi "Victoria Falls Zimbabwe, maporomoko makubwa kuliko yote duniani lakini kumbe hapa ni tofauti sana" amesema bongozozo
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika katika Pori hilo, bongozozo amefurahishwa na mazao mapya ya Utalii yaliyopo katika hifadhi hiyo na kutaja "TAWA mserereko" kama zao la utalii linalomfanya mtalii kuburudika awapo katika hifadhi hiyo kwani humfanya mtalii kuteleza katika maji jambo linaloleta furaha Kwa mtalii

Aidha amempongeza mwongoza utalii wa hifadhi hiyo Askari Mhifadhi daraja la tatu Leonard Nsajigwa Kwa uelewa mkubwa juu ya vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo na utopezi wake katika kuvielezea
Pia bongozozo ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia uongozi wa Pori hilo kwa utunzaji mzuri wa mazingira na hivyo kuifanya hifadhi kuwa safi pasina utupaji hovyo wa taka, jambo ambalo amedai linavutia sana watalii

Awali akiwakaribisha watalii katika hifadhi hiyo, Kamishna wa Uhifadhi Msaidizi - Utalii Kanda ya Nyanda za Juu kusini Martha Msemo amesema Pori la Akiba Mpanga/Kipengere limesheheni vivutio mbalimbali ambavyo vinapelekea utalii wa kihistoria, utamaduni na mandhari kufanyika hifadhini humo.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuboresha miundombinu ya Utalii katika Pori hilo hususan malazi Kwa wageni na watalii mbalimbali wanaotembelea Pori hilo.

Akielezea umuhimu wa Pori hilo, Martha Msemo amesema Pori la Akiba Mpanga/Kipengere lina vyanzo vingi vya maji ambayo kiikolojia yanatumika katika ikolojia ya Ruaha - Rungwa, na pia maji hayo hutumika kuwasaidia wananchi katika shughuli za kilimo Cha umwagiliaji pamoja na kuwa chanzo muhimu cha maji katika bwawa la Nyerere
Zaidi ya Watalii 200 wameadhimisha siku ya maporomoko ya maji duniani pamoja na kutalii na balozi wa utalii nchini, bongozozo katika Pori hilo la Akiba.



