BODI YA WAKURUGENZI YA TAWA YATETA NA MAAFISA NA ASKARI

BODI YA WAKURUGENZI YA TAWA YATETA NA MAAFISA NA ASKARI

Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), leo Februari 20,2026, imefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mej.Jen (Mst) Hamis Semfuko, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Dkt. Simon Mduma amesema lengo kubwa la ziara  ya Bodi ya Wakurugenzi ni kujitambulisha pamoja na kufanya kikao na Maafisa na Askari.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya Bodi zilizomaliza muda wake, Dkt. Mduma amesema Bodi za Wakurugenzi zilizopita zilifanya mambo mengi mazuri na ya kupongezwa yakiwemo kuimarisha ulinzi wa wanyamapori, kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza pato la Serikali kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwemo uwekezaji mahiri (SWICA) ambavyo vimeifikisha TAWA hapa ilipo leo.


Vilevile, Dkt. Mduma amesema Bodi ya Nne imejipanga kuhakikisha TAWA inazidi kukua na kupaa zaidi katika nyanja zote za kiutendaji ikiwemo kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato yatakayoisaidia TAWA kuweza kujitegemea.


Pia, kuendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo ya hifadhi na kuendelea kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo teknolojia katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Sambamba na hilo, Dkt. Mduma amewataka Maafisa na Askari kuendelea kuzingatia sheria, haki, uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu, na ameongeza kuwa Bodi ya Nne itahakikisha inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi.


Awali, akiwakaribisha wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Yussuf Kabange amesema kwa upande wa rasilimali watu, kwa mwaka wa fedha 2025/26, Serikali imetoa vibali vya kuajiri Askari wa Wanyamapori takribani 551 ambao wataenda kuongeza nguvu katika ulinzi wa rasilimali wanyamapori.

Aidha, amesisitiza kuwa Menejimenti inaendelea kuhakikisha kuwa Maafisa na Askari wanaendelea kupata stahiki zao ili kuendelea kuimarisha morali katika utekelezaji wa majukumu.

Hii ni ziara ya kwanza ya kikazi ya Bodi ya Wakurugenzi kutembelea ofisi za TAWA Makao Makuu tangu ilipozinduliwa rasmi Jijini Arusha mnamo Januari 9,2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt Ashatu Kijaji.