NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI INAYOSIMAMIWA NA TAWA

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI INAYOSIMAMIWA NA TAWA

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii Juma Mkomi ameeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19 katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.

Naibu Katibu Mkuu ameyasema hayo leo Novemba 10, 2022, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na TAWA katika Pori la Akiba Wamimbiki lililopo katika Mikoa ya Morogoro na Pwani.

"Niwapongeze Kwa usimamizi mzuri wa fedha hizi zilizoletwa na Serikali, nimeona zinafanya kazi ambayo ilikusudiwa" amesema Mkomi.

"Tuongeze jitihada za usimamizi mzuri wa hii miradi ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa, sambamba na hilo hakikisheni mnatenga bajeti ili miradi hii iwe inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili isipoteze ubora wake hususani barabara" amesisitiza Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi.

Ziara hii imehusisha ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 47.2, lango kuu la kuingilia wageni na mabanda ya kupumzikia wageni ambayo yote imekamilika kwa asilimia mia moja ( 100%).Kwa upande wake, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi - TAWA , Mlage Kabange amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo, ambazo zimeisaidia TAWA kuboresha miundombinu ya utalii katika maeneo inayoisimamia.

Vilevile amemshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa ujio wake na amemhakikishia utekelezaji wa maagizo na ushauri alioutoa.