KAIMU KAMISHNA WA UHIFADHI TAWA AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAANDALIZI YA BAJETI YA TAWA

KAIMU KAMISHNA WA UHIFADHI TAWA AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAANDALIZI YA BAJETI YA TAWA

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda leo Februari 3, 2023 amefungua rasmi kikao kazi Cha Maandalizi ya  bajeti ya TAWA Kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa TAFORI mjini Morogoro.


Akizungumza Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Kamishna Mabula amesema Bodi na Menejimenti ya TAWA Ina matarajio makubwa kuwa bajeti inayoandaliwa itaweka misingi imara katika kuhakikisha malengo ya Mpango Mkakati ambayo yamezingatia ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26 yanatimia.


Kamishna Mabula amebainisha kuwa vipaumbele vya TAWA katika mpango wa bajeti hiyo vimejikita katika ulinzi wa rasilimali za Wanyamapori na malikale ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vitendea kazi, kuimarisha miundombinu, usimamizi wa magari na mitambo.

Pia Udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu, utatuzi wa migogoro kati ya hifadhi na jamii, kuimarisha Utalii na kuongeza mapato pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi ambavyo Kwa ujumla vinalenga kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.

Aidha Kamishna Mabula amewaelekeza makamanda wote wa Kanda Kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza idadi ya watalii na mapato katika Kila Pori na Maeneo ya Malikale, kusimamia nidhamu ya matumizi ya vitendeakazi hususan magari na kuepusha kuzalisha madeni.

Pia ameelekeza kuimarisha miundombinu ya Utalii ikiwa ni pamoja na kukuza Utalii wa fukwe na kuhakikisha suala la kuingiza mifugo hifadhini linadhibitiwa kikamilifu katika Kanda zote.

Hali kadhalika, Kamishna Mabula amempongeza Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Meneja Pori la Akiba Uwanda Kwa kuendelea kuongeza mapato ambapo hadi kufikia Disemba 2022 Pori la Uwanda lilikusanya jumla ya Shillingi Millioni 823.9 kutoka katika eneo lake na hivyo kusisitiza makamanda wote kuongeza ubunifu Ili kuongeza mapato katika maeneo yao.