Skip to main content

MWONGOZO WA SHUGHULI ZA UFUGAJI NYUKI KATIKA MAPORI YA AKIBA, MAPORI TENGEFU NA ARDHIOEVU WA MWAKA 2021

MWONGOZO WA SHUGHULI ZA UFUGAJI NYUKI KATIKA MAPORI YA AKIBA, MAPORI TENGEFU NA ARDHIOEVU WA MWAKA 2021

____________

SEHEMU YA KWANZA

1.1 Utangulizi:

Ibara ya 27(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inampa kila mtu wajibu wa kulinda maliasilia zote za nchi. Aidha, Ibara ya 9(c) ya Katiba inaruhusu rasilimali za nchi kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote. Kutokana na msingi huo wa kikatiba, Sera ya Taifa ya Wanyamapori ya mwaka 2007 inalenga kuhakikisha kuwa kuna uhifadhi endelevu wa rasilimali za wanyamapori na ardhioevu. Katika kufikia lengo hilo, Sera inahimiza uhifadhi, usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori bila kuathiri mazingira kwa madhumuni ya kukabiliana na umasikini. Katika kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, Sera inasisitiza, pamoja na mambo mengine, kuongeza uzalishaji katika sekta nyingine za kiuchumi.

Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 inasisitiza kuwepo kwa makubaliano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania na vikundi vya wafugaji wa nyuki yanayoruhusu ufugaji nyuki katika maeneo yaliyohifadhiwa. Sera hiyo inaelekeza kuwepo kwa uratibu wa pamoja kati ya Mamlaka na taasisi inayohusika na usimamizi wa ufugaji nyuki kwa masuala yanayohusu ufugaji nyuki katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Kwa mujibu wa Sera hiyo, makubaliano kati ya Mamlaka na vikundi vya wafugaji nyuki ni mkakati wa kuhakikisha kuwa kuna uhifadhi endelevu kupitia ushiriki wa wananchi katika kusimamia na kutumia maliasilia za nchi. Vilevile, Sera inaainisha kuwepo kwa utaratibu wa kugawana faida kati ya Mamlaka na wafugaji wa nyuki wanaofuga katika maeneo yaliyohifadhiwa.